Joel 2

Jeshi La Nzige


1 aPigeni tarumbeta katika Sayuni;
pigeni mbiu katika mlima wangu mtakatifu.
Wote waishio katika nchi na watetemeke,
kwa kuwa siku ya Bwana inakuja. Iko karibu,

2 bsiku ya giza na huzuni,
siku ya mawingu na utusitusi.
Kama mapambazuko yasambaavyo
toka upande huu wa milima
hata upande mwingine
jeshi kubwa na lenye nguvu linakuja.
Jambo kama hili halijakuwepo tangu zamani
wala halitakuwepo tena kamwe
kwa vizazi vijavyo.

3 cMbele yao moto unateketeza,
nyuma yao miali ya moto
inawaka kwa nguvu.
Mbele yao nchi iko kama bustani ya Edeni,
nyuma yao ni jangwa lisilofaa:
hakuna kitu kinachowaepuka.

4 Wanaonekana kama farasi;
wanakwenda mbio
kama askari wapanda farasi.

5 dWanatoa sauti kama magari ya vita,
wanaporukaruka juu ya vilele vya milima,
kama mlio wa miali ya moto ilayo mabua,
kama jeshi kubwa lililojipanga kwa ajili ya vita.


6 eWanapoonekana, mataifa yanakuwa katika maumivu makuu;
kila uso unabadilika rangi.

7 fWanashambulia kama wapiganaji wa vita;
wanapanda kuta kama askari.
Wote wanatembea katika safu,
hawapotoshi safu zao.

8 Hakuna anayemsukuma mwenzake;
kila mmoja anakwenda mbele moja kwa moja.
Wanapita katika vizuizi
bila kuharibu safu zao.

9 gWanaenda kasi kuingia mjini;
wanakimbia ukutani.
Wanaingia ndani ya nyumba;
kwa kuingilia madirishani kama wevi.


10 hMbele yao dunia inatikisika,
anga linatetemeka,
jua na mwezi vinatiwa giza,
na nyota hazitoi mwanga wake tena.

11 i Bwana anatoa mshindo wa ngurumo
mbele ya jeshi lake;
majeshi yake hayana idadi,
ni wenye nguvu nyingi
wale ambao hutii agizo lake.
Siku ya Bwana ni kuu,
ni ya kutisha.
Ni nani anayeweza kuistahimili?

Rarueni Mioyo Yenu


12 j“Hata sasa,” asema Bwana,
“nirudieni kwa mioyo yenu yote,
kwa kufunga, kwa kulia na kuomboleza.”


13 kRarueni mioyo yenu
na siyo mavazi yenu.
Mrudieni Bwana, Mungu wenu,
kwa maana yeye ndiye mwenye neema
na mwingi wa huruma,
si mwepesi wa hasira, ni mwingi wa upendo,
huona huruma, hujizuia kuleta maafa.

14 lNi nani ajuaye? Yeye aweza kugeuka na kuwa na huruma
na kuacha baraka nyuma yake:
sadaka za nafaka na sadaka za vinywaji
kwa ajili ya Bwana Mwenyezi Mungu wenu.


15 mPigeni tarumbeta katika Sayuni,
tangazeni saumu takatifu,
liiteni kusanyiko takatifu.

16 nWakusanyeni watu,
wekeni wakfu kusanyiko;
waleteni pamoja wazee,
wakusanyeni watoto,
wale wanyonyao maziwa.
Bwana arusi na atoke chumbani mwake
na bibi arusi naye atoke katika chumba chake.

17 oMakuhani, ambao wanahudumu mbele za Bwana,
na walie katikati ya ukumbi
wa Hekalu na madhabahu.
Waseme, “Wahurumie watu wako, Ee Bwana.
Usifanye urithi wako kitu cha kudharauliwa,
neno la dhihaka kati ya mataifa.
Kwa nini wasemezane miongoni mwao,
‘Yuko wapi Mungu wao?’ ”

Jibu La Bwana


18 pKisha Bwana atakuwa na wivu kwa ajili ya nchi yake
na kuwa na huruma juu ya watu wake.

19 q Bwana atawajibu:
“Ninawapelekea nafaka,
mvinyo mpya na mafuta,
vya kuwatosha ninyi
hadi mridhike kabisa;
kamwe sitawafanya tena
kitu cha kudharauliwa na mataifa.


20 r“Nitafukuza jeshi la kaskazini likae mbali nanyi,
nikilisukuma ndani ya jangwa,
askari wa safu za mbele wakienda
ndani ya bahari ya mashariki
na wale wa safu za nyuma
katika bahari ya magharibi.
Uvundo wake utapaa juu;
harufu yake itapanda juu.”

Hakika ametenda mambo makubwa.

21 sUsiogope, ee nchi;
furahi na kushangilia.
Hakika Bwana ametenda mambo makubwa.

22 tMsiogope, enyi wanyama pori,
kwa kuwa mbuga za malisho yenu
zinarudia ubichi.
Miti nayo inazaa matunda,
mtini na mzabibu inatoa utajiri wake.

23 uFurahini, enyi watu wa Sayuni,
shangilieni katika Bwana Mwenyezi Mungu wenu,
kwa kuwa amewapa mvua za vuli
kwa kipimo cha haki.
Anawapelekea mvua nyingi,
mvua ya vuli na ya masika, kama mwanzoni.

24 vSakafu za kupuria zitajaa nafaka,
mapipa yatafurika mvinyo mpya na mafuta.


25 w“Nitawalipa kwa ajili ya miaka ile iliyoliwa na nzige:
parare, madumadu na tunutu,
jeshi langu kubwa ambalo
nililituma katikati yenu.

26 xMtakuwa na wingi wa vyakula mpaka mshibe,
na mtalisifu jina la Bwana Mwenyezi Mungu wenu,
ambaye amefanya maajabu kwa ajili yenu;
kamwe watu wangu hawataaibishwa tena.

27 yNdipo mtakapojua kwamba mimi niko katika Israeli
kwamba mimi ndimi Bwana Mwenyezi Mungu wenu,
na kwamba hakuna mwingine;
kamwe watu wangu hawataaibika tena.

Siku Ya Bwana


28 z“Hata itakuwa, baada ya hayo,
nitamimina Roho wangu juu ya wote wenye mwili.
Wana wenu na binti zenu watatabiri,
wazee wenu wataota ndoto,
na vijana wenu wataona maono.

29 aaHata juu ya watumishi wangu, wanaume kwa wanawake,
katika siku zile nitamimina Roho wangu.

30 abNami nitaonyesha maajabu katika mbingu
na duniani:
damu, moto na mawimbi ya moshi.

31 acJua litageuzwa kuwa giza
na mwezi kuwa mwekundu kama damu,
kabla ya kuja siku ya Bwana
ile kuu na ya kutisha.

32 adNa kila mtu atakayeliitia
jina la Bwana ataokolewa.
Kwa maana juu ya Mlima Sayuni na katika Yerusalemu
kutakuwepo wokovu,
kama Bwana alivyosema,
miongoni mwa walionusurika
ambao Bwana awaita.
Copyright information for SwhKC